Msanii wa Korea Kusini Moon Tae-il, anayefahamika kama Taeil, ambaye alikuwa mwanachama wa kundi la K-pop NCT, amehukumiwa miaka mitatu na nusu jela kwa kosa la ubakaji.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 31, pamoja na wenzake wawili wanaojulikana kwa majina ya Lee na Hong, walikiri mnamo Juni kwamba walishirikiana kumbaka msafiri mwanamke kutoka China.
Jaji mmoja wa jiji la Seoul alieleza kuwa kosa hilo ni “zito sana“, lakini akawapa nusu ya adhabu ya miaka 7 iliyokuwa imependekezwa na waendesha mashtaka, kwa kuzingatia kuwa hilo lilikuwa kosa lao la kwanza, kwa mujibu wa ripoti za BBC.
Mahakama pia iliamuru wanaume hao watatu kuhudhuria masomo ya saa 40 ya matibabu ya tabia ya wahalifu wa kingono.

Shirika la burudani la SM Entertainment, lililokuwa likisimamia kazi za Moon, lilitangaza kuwa aliondoka katika kundi la NCT mwezi Oktoba 2024, baada ya miaka 8 ya uanachama.
SM Entertainment lilieleza:
“Kutokana na uzito wa suala hili, tumeamua kwamba hawezi tena kuendelea na shughuli za kikundi.”

Taeil alianza muziki wake na kundi la NCT U mwaka 2016, kisha akaingia NCT 127.


