Chama cha Mpira wa Kikapu cha Marekani (NBA) kimetangaza kuiondoa timu ya APR Basketball katika mashindano ya Basketball Africa League (BAL) ya mwaka 2026, kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Serikali ya Marekani dhidi ya Jeshi la Rwanda.
Uamuzi huo umethibitishwa na NBA katika majibu yake kwa maseneta wawili wa Marekani waliokuwa wameiomba kueleza sababu za kuendelea kushirikiana na timu inayofadhiliwa na Jeshi la Rwanda.
Katika barua ya tarehe 23 Oktoba 2026, Seneta Jeffrey Merkley wa Chama cha Democratic na Marsha Blackburn wa Chama cha Republican waliitaka NBA kupitia upya uhusiano wake na Rwanda. Waliishutumu kwa kuunga mkono shughuli zinazoweza kutafsiriwa kuwa ni matumizi ya michezo kuboresha taswira ya nchi kimataifa, wakati kukiwa na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.
Maseneta hao walihoji NBA kuhusu vigezo inavyotumia kuamua kupokea fedha kutoka kwa serikali zinazotuhumiwa kukiuka haki za binadamu.
Katika majibu yake, Makamu wa Rais wa NBA, Mark Tatum, alisema kuwa timu ya APR Basketball iliondolewa katika mashindano ya BAL kufuatia vikwazo ambavyo Marekani iliiwekea Jeshi la Rwanda mwezi Machi 2026.
Aliongeza kuwa timu hiyo itaendelea kutoruhusiwa kushiriki mashindano hayo kwa muda wote ambao vikwazo hivyo vitakuwa vinaendelea kutumika.
Mwezi Machi 2026, Serikali ya Marekani iliweka vikwazo dhidi ya Jeshi la Rwanda.
Hivi karibuni, Marekani pia iliweka vikwazo dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda, ikiishutumu kwa kuunga mkono kundi la M23, ambalo limeteka maeneo mbalimbali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha mara kwa mara tuhuma za kuliunga mkono kundi hilo.
APR Basketball ni mojawapo ya timu kubwa za mpira wa kikapu nchini Rwanda. Timu hiyo ilishiriki mashindano ya Basketball Africa League mwaka 2024 na 2025.
Katika mashindano ya mwaka 2026, APR Basketball imechukuliwa nafasi yake na RSSB Tigers, ambayo pia inaiwakilisha Rwanda.

