Jeshi la Nigeria limetangaza kuwakamata wanajeshi na maafisa wa polisi zaidi ya 30 waliotuhumiwa kuuza silaha kwa makundi ya waasi na magaidi.
Msemaji wa jeshi la Nigeria, Ademola Owolana, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako unaoendelea tangu mwezi Agosti mwaka jana.
Tukio hili linajiri wakati ambapo Nigeria inakabiliwa na changamoto kubwa za usalama kutokana na makundi yenye silaha kama Boko Haram ambayo yamekuwa yakitishia usalama wa Kaskazini mwa nchi kwa zaidi ya miaka 15.
Inasemekana kuwa zaidi ya asilimia 20 ya silaha zinazotumiwa na makundi haya zinapatikana kutoka kwa polisi na wanajeshi wa Nigeria.
Waliokamatwa ni pamoja na wanajeshi 18, polisi 15 na raia 8 — akiwemo kiongozi wa kijadi — wote wakishtakiwa kwa kuhusika na biashara haramu ya silaha.
Jeshi pia limetangaza kuwa uchunguzi unaendelea katika majimbo 11 ya Nigeria ili kuwabaini na kuwakabili wengine walio nyuma ya mtandao huu haramu wa silaha.


