Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa nchini Rwanda inamfuatilia mwanaume mkazi Wilayani Nyanza, kusini mwa Rwanda, anayeshukiwa kutoa Frw 300,000 kwa mtu mwingine ili amsaidie kumuua mdogo wake, ingawa mwanaume huyo anakanusha mashtaka yanayomkabili.
Mnamo tarehe 6 Oktoba 2026, katika Mahakama ya Mwanzo ya Busasamana, Wilaya ya Nyanza, kulisikilizwa kesi kuhusu maombi ya kuwekwa rumande kwa muda kwa Shumbusho Marc na Habimana Schadrack, anayejulikana kwa jina la Kazungu, ambaye ni kaka mkubwa wa marehemu Habanabashaka Janvier.
Upande wa mashtaka unasema kwamba katika usiku wa manane wa tarehe 17 Septemba 2026, katika Kijiji cha Nyamiyaga, Kitongoji cha Gacu, Sekta ya Rwabicuma, Habanabashaka alikutwa amefariki ndani ya mtaro, bila kuwa na jeraha lolote lililoonekana mwilini.
Mwakilishi wa upande wa mashtaka alisema: “Upelelezi ulianza na kubaini kwamba marehemu aliuawa na Shumbusho akishirikiana na kaka yake aitwaye Habimana.”
Upande wa mashtaka unasema kwamba kabla ya kifo chake, Habanabashaka alikuwa amekunywa pombe pamoja na Shumbusho katika baa, na baadaye wakaondoka pamoja kuelekea nyumbani. Wakiwa njiani, inadaiwa Shumbusho alishirikiana na Habimana, kaka wa marehemu, na wakamnyonga hadi kufariki.
Umeendlea kuambia koti kwamba Habimana alikuwa amemuahidi Shumbusho Frw 300,000 kama malipo ya kumsaidia kumuua Habanabashaka.
Mwendesha Mashtaka alisema: “Marehemu Habanabashaka alikuwa na mgogoro na kaka yake kuhusu suala la marehemu kuishi katika nyumba iliyokarabatiwa na kaka yake.”
Upande wa mashtaka unasema unategemea maelezo yaliyotolewa na Shumbusho, ambapo alimhusisha Habimana na mauaji hayo, huku wakisubiri ushahidi mwingine wa kisayansi na uchunguzi ukiendelea. Uliomba washukiwa wote wawili kuwekwa rumande kwa muda wa siku 30.
Mbele ya mahakama, Shumbusho alikiri kumuua Habanabashaka na kuomba msamaha. Hata hivyo, alisema kwamba maelezo aliyotoa kwa Upelelezi na upande wa mashtaka, akimtuhumu Habimana kuwa walishirikiana katika mauaji hayo, hayakuwa ya kweli.
Alisema kwamba alipokuwa katika Kituo cha Polisi cha RIB cha Nyagisozi, alisema kuwa alishirikiana na Habimana, wakati ukweli ni kwamba haikuwa hivyo.
Jaji alimuuliza Shumbusho kuhusu alichowaambia wenzake waliokuwa wamefungwa pamoja naye baada ya kufikishwa rumande. Shumbusho alijibu: “Nilisema kwamba tulimuua mtu, lakini hakuna aliyenipiga.”
Shumbusho alisema kwamba alimuua Habanabashaka baada ya kutokea mzozo uliosababishwa na pombe ya kienyeji waliyokuwa nayo wakati wakielekea nyumbani. Alikiri kwamba ndiye aliyemnyonga marehemu akiwa peke yake, bila kusaidiwa na mtu mwingine.
Alisema: “Nilipofika katika Kituo cha RIB cha Busasamana, ndipo wenzangu tuliokuwa tumefungwa pamoja walinishauri kwamba sikupaswa kuendelea kumtuhumu mtu ambaye hakujua chochote kuhusu kifo cha marehemu.”
Habimana Schadrack, kwa upande wake, alikanusha kuhusika na kifo cha mdogo wake, akisema kwamba alifahamu kuhusu kifo chake asubuhi, baada ya kuitwa na kuambiwa kwamba alikuwa amepatikana amefariki.
Alisema: “Waliniita ili niende kutoa taarifa, ndipo wakaniweka kizuizini.”
Me Célèstin Nshimiyimana, wakili wa Habimana Schadrack, aliiambia mahakama kwamba hakuna sababu za msingi za kumweka mteja wake rumande kwa muda.
Alisema kwamba Shumbusho ndiye anayepaswa kuwajibishwa kwa kifo cha Habanabashaka, kwa kuwa yeye mwenyewe amekiri kuwa ndiye aliyemuua.
Alisema: “Kauli aliyoitoa hapa mahakamani kwamba mteja wangu anasingiziwa ndiyo inapaswa kupewa uzito.”
Me Nshimiyimana pia aliiambia mahakama kwamba hata wazazi wa marehemu hawakuwahi kumshitaki Habimana Schadrack, kwa sababu walijua kwamba hakuwa na tatizo lolote na mdogo wake.
Jaji alisema: “Usisisitize hilo suala la mzazi. Badala ya kupoteza watoto wawili, angekuwa amempoteza mmoja na mwingine akabaki. Mzazi hawezi kufurahia mtoto wake kufariki na mwingine pia kufungwa.”
Me Célèstin Nshimiyimana aliiomba mahakama kumuachilia mteja wake, akisema kwamba hakuna sababu za msingi za kumweka rumande kabla ya kesi kusikilizwa kikamilifu.
Jaji alisema kwamba uamuzi wa mahakama utatangazwa tarehe 9 Oktoba 2026.

