Wanasayansi wamesema kuwa chombo cha anga cha Parker kimeweza “kukigusa” Jua kwa kufika umbali wa kilomita milioni 6.1 kutoka kwenye uso wake—umbali wa karibu zaidi kuwahi kufikiwa na chombo chochote cha kibinadamu.
Tarehe 24 Desemba 2024, Parker ilipita karibu sana na Jua kwa kasi ya kushangaza ya km 700,000 kwa saa. Ina kinga maalum ya kaboni inayostahimili joto kali la hadi nyuzi joto 1,400°C, ikilinda kamera na vifaa vyake dhidi ya joto hilo kali.
Dhamira ya Parker
Chombo cha Parker kilitumwa angani tarehe 12 Agosti 2018 kwa lengo la kukichunguza Jua kwa karibu. Kinachunguza tabaka la nje la anga ya Jua lijulikanalo kama corona, upepo wa jua wenye nguvu, na nishati inayotoka kwenye Jua.
Parker ilipambana na nguvu ya mvutano mkubwa wa Jua unaosababisha kila kitu karibu nacho kuzunguka kwa kasi sana. Iliweza kufikia kasi ya km 692,000 kwa saa—kasi ya juu zaidi kuwahi kufikiwa na chombo chochote kilichotengenezwa na binadamu.
Miongoni mwa malengo ya kisayansi ya Parker ni kuelewa kwa nini tabaka la corona lina joto zaidi kuliko uso wa Jua, kuchunguza chanzo cha upepo wa jua, na kuelewa jinsi chembechembe za nishati husukumwa kwa kasi kubwa hivyo.
Chombo hiki kilipewa jina la mwanafizikia wa Marekani Eugene Parker, aliyefariki mwezi Machi 2022.


