Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa anatarajia kupokea ndege ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 400 za Kimarekani (sawa na Shilingi bilioni 536 za Rwanda), iliyotolewa kama zawadi na familia ya kifalme ya Qatar.
Ndege hiyo aina ya Boeing 747-8 inaweza kutumika kama “Air Force One” kwa muda, kufuatia ucheleweshaji wa Boeing katika kutoa ndege mpya za rais.
Zawadi hiyo imekuja wakati utawala wa Trump ukikumbwa na changamoto ya kucheleweshwa kwa ndege mpya, na Qatar ikaamua kuingilia kati kama msaada wa haraka.
Kupitia Truth Social, Trump aliandika: “Wizara ya Ulinzi inapokea ndege mpya, bure, waziwazi. Wademocrat wamekasirika—wanataka tutumie pesa nyingi. Ni fedheha.”
Wachambuzi wa usalama wameonya kuwa zawadi ya aina hii si ya kawaida katika diplomasia na inaweza kuwa na hatari kama kuwekwa kwa vifaa vya upelelezi ndani ya ndege. Baadhi wanaiona kama ishara ya urafiki wa kutatanisha kati ya Trump na Qatar.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Qatar alisema kuwa “mazungumzo bado yanaendelea kati ya pande zote mbili” na “hakuna uamuzi wa mwisho ambao umefikiwa bado.”


