José Mujica, aliyejulikana duniani kama “rais maskini zaidi duniani”, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89. Mwanasiasa huyu kutoka Uruguay na aliyewahi kuwa mpiganaji wa msituni, aliongoza nchi yake kati ya mwaka 2010 hadi 2015.
Mujica aliheshimika kwa maisha yake rahisi na kwa kukataa kujilimbikizia mali, jambo lililomtofautisha na viongozi wengi duniani.
Rais wa sasa wa Uruguay, Yamandú Orsi, alithibitisha kifo chake kupitia akaunti yake ya X (zamani Twitter), akiandika: “Asante kwa yote uliyotupa na kwa upendo wako mkubwa kwa watu wako.”
Ingawa sababu rasmi ya kifo haijatajwa, Mujica alikuwa akisumbuliwa na saratani ya koo kwa muda.
Alivuma dunia nzima kwa kuishi maisha ya kawaida alipokuwa rais: alikataa kuishi katika Ikulu na badala yake aliendelea kuishi katika nyumba ndogo ya vijijini pamoja na mkewe. Alikuwa akitumia gari la zamani aina ya Volkswagen Beetle ya mwaka 1987, na mara nyingi alivaa nguo za kawaida. Alikuwa akitoa mshahara wake kwa taasisi za misaada.
Hali hiyo ilimfanya aitwe “rais maskini zaidi duniani”, ingawa yeye alikana jina hilo akisema: “Maskini wa kweli ni wale wanaotamani kila wakati kuwa na zaidi.”
Katika miaka ya 1960, Mujica alikuwa mwanachama wa kundi la wapiganaji wa msituni wa Tupamaros, lililotaka mabadiliko ya kisiasa. Alikamatwa mara nne na kufungwa kwa zaidi ya miaka 14, na mara moja alipigwa risasi sita. Aliwahi kutoroka gerezani kupitia handaki akiwa na wapiganaji wengine 105.
Alisema: “Siku niliyoachiwa huru ilikuwa yenye furaha kuliko hata siku nilipochaguliwa kuwa rais.”
Mujica alichaguliwa kuwa rais mwaka 2010 akiwa na miaka 74. Wakati wake madarakani, uchumi wa Uruguay ulikua, umasikini ulipungua, na alipitisha sheria za kimapinduzi kuhusu uavyaji mimba, ndoa za jinsia moja, na udhibiti wa bangi.
Ingawa alikosolewa kwa matumizi ya fedha za umma na changamoto katika elimu, hakuwahi kushutumiwa kwa ufisadi au kuvuruga demokrasia.
Katika mahojiano aliyofanya na BBC mwezi Novemba 2024, Mujica alisema: “Kifo hakiwezi kuepukwa. Labda ni kama chumvi ya maisha.” Alikuwa ametangaza kuwa ana saratani, lakini aliendelea kuikabili kwa ujasiri.
Alijiondoa rasmi katika siasa mwaka 2020, lakini aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa nyumbani na kimataifa.
Yamandú Orsi, mrithi wake wa kisiasa, alichaguliwa kuwa rais mwaka 2024, akiendeleza urithi wa Mujica katika siasa na maisha ya taifa.


