Rais wa Kenya William Ruto amemfuta kazi Dkt. Swarup Mishra kutoka nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kenya BioVax, kufuatia tuhuma za kuhusika na biashara haramu ya viungo vya binadamu kupitia hospitali zake za Mediheal.
Taarifa hiyo ilitolewa Ijumaa, tarehe 4 Julai 2025, kupitia tangazo rasmi la serikali lililosainiwa na Rais Ruto mwenyewe.
Dkt. Mishra alikuwa ameteuliwa Desemba 2024, lakini alisimamishwa kazi hivi karibuni ili kuruhusu uchunguzi wa kina kuhusiana na tuhuma hizo nzito.
Rais Ruto alimchagua Dkt. Charles Githinji kuchukua nafasi hiyo. Dkt. Githinji alikuwa afisa mwandamizi katika Bodi ya Kudhibiti Dawa na Sumu ya Kenya.
Dkt. Mishra, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kesses, amekuwa akihusishwa mara kwa mara na biashara haramu ya figo na viungo vingine vya binadamu, jambo lililosababisha taharuki kubwa miongoni mwa wananchi na wataalamu wa afya.


