Jumapili, tarehe 1 Juni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alikutana na Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani, katika ziara rasmi ya kikazi nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, viongozi hao wawili walijadili jinsi ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa yao.
Taarifa hiyo ilisema: “Pande zote mbili zilijadili uhusiano wa ushirikiano kati ya nchi hizo na njia za kuuendeleza na kuutia nguvu.”
Qatar pia inahusika moja kwa moja katika juhudi za kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kusuluhisha pande zinazohusika, zikiwemo Rwanda na DRC. Masuala haya yalijadiliwa katika kikao chao huku mazungumzo yakiendelea.
Qatar ilisema: “Pia walizungumzia juhudi za kusuluhisha mzozo kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na masuala mengine yenye maslahi ya pamoja.”
Ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na Qatar ni wa kiwango cha juu, ukihusisha sekta mbalimbali kama anga, ulinzi na usalama, pamoja na teknolojia ya mawasiliano (ICT).
Qatar Airways imewekeza katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Bugesera wenye thamani ya dola bilioni 2, ambao unatarajiwa kukamilika mwaka wa 2028.
Tarehe 12 Februari, Rais Kagame alikutana na Emir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani, mjini Doha.
Qatar pia imeidhinisha mkataba wa makubaliano ya kuondoa visa kwa raia wa mataifa yote mawili wenye pasi za kawaida.
Mkataba huu uliidhinishwa tarehe 12 Februari. Kabla ya hapo, raia wa Rwanda waliruhusiwa kuingia Qatar bila visa kwa kipindi cha siku 30.

