Ripoti inayoitwa Country Policy and Institutional Assessment (CPIA) inategemea vigezo vinne muhimu: usimamizi wa uchumi, sera za mageuzi ya sekta za uchumi, sera zinazolenga usawa na ustawi wa jamii, pamoja na usimamizi wa taasisi na mashirika ya serikali.
Rwanda imehifadhi alama ilizopata mwaka 2024. Alama hizo zinaiweka katika nafasi nzuri ya kupata mikopo ya muda mrefu yenye riba nafuu, pamoja na misaada inayolenga maendeleo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda imepata alama 4.2, ambazo zinazidi kwa pointi 1.1 kiwango cha alama 3.1 kinachowekwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA), ambalo ni tawi la Benki ya Dunia linalosaidia nchi zinazoendelea, kama kigezo cha nchi kupata mikopo au misaada.
Miongoni mwa vigezo vilivyotathminiwa, Rwanda ilipata alama za juu zaidi katika eneo la sera zinazolenga usawa na ustawi wa jamii, ambapo ilipata alama 4.5.
Ripoti inaonesha kuwa Rwanda ina sera na programu zinazolenga kuhakikisha kuwa maendeleo yanawafikia watu wote na kuwapa watu wa makundi mbalimbali fursa sawa za kujiendeleza.
Pia inaonesha hatua zilizopigwa katika kuandaa programu na sera zinazolenga kupunguza umaskini. Alama ya jumla ya 4.2 ambayo Rwanda ilipata inaonesha juhudi zilizowekwa katika kuboresha sera na utendaji wa taasisi, jambo linalosaidia matumizi bora ya mikopo na misaada inayotolewa na taasisi za kimataifa za fedha.
Licha ya Rwanda kufanya vizuri kwa ujumla, ripoti hiyo inaonesha kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika usimamizi wa taasisi na mashirika ya serikali.
Katika kipimo hiki, Rwanda ilipata alama 3.9, ambazo ndizo za chini zaidi ikilinganishwa na alama ilizopata katika vigezo vingine vitatu vilivyotathminiwa.
Ripoti inasisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika mageuzi ya utendaji wa taasisi hizo ili kuhakikisha kuwa sera zinazowekwa zinatekelezwa ipasavyo na kuleta matokeo yanayoonekana.
Nchi zinazofuatia Rwanda ni Côte d’Ivoire, iliyopata alama 4.0; Benin na Cabo Verde, ambazo kila moja ilipata alama 3.9; pamoja na Kenya na Togo, ambazo kila moja ilipata alama 3.8.


