Taarifa kutoka kwa vyombo vya usalama nchini Uganda zinaeleza kuwa serikali inazingatia kulifuta chama cha upinzani National Unity Platform (NUP) kutokana na hofu inayoongezeka kuwa chama hicho kinajihusisha na mienendo ya kijeshi na shughuli zinazotishia usalama wa taifa. Hatua hii inakuja wakati Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Suala hili lilijadiliwa kwa kina katika mkutano wa juu wa jeshi la UPDF ulioongozwa na Rais Yoweri Museveni katika makaazi yake mjini Entebbe.
Kwa mujibu wa Chimpreports, wakuu wa usalama walimweleza Rais Museveni kuhusu hofu yao kwamba NUP inaharibu vijana kifikra na kutovumilia maoni tofauti ya kisiasa.
Baada ya mkutano huo, Rais Museveni alitoa wito wa kulinda nafasi ya demokrasia dhidi ya vitisho vya kisiasa.
Alisema: “Nimesisitiza kuwa Uganda inahitaji demokrasia yenye nidhamu. NRM inaunga mkono demokrasia ya nidhamu, si vurugu wala lugha za matusi.”
“Wanasiasa wanaowatisha wananchi lazima wakome! Hii si njia ya Afrika. Vyombo vya usalama vimechukua hatua, na suala hili litapatiwa suluhisho.”
Aliwasihi vijana kujifunza uzalendo na kuiga maadili ya chama cha NRM, huku akionya dhidi ya kushiriki vurugu kwa kivuli cha harakati za kisiasa.
Kauli zake zinakuja wakati ambapo wanachama na viongozi kadhaa wa NUP wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa mazito.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Eddie Mutwe, mlinzi wa muda mrefu wa Bobi Wine, ambaye amefikishwa mahakamani Masaka kwa kosa la wizi na kupelekwa gerezani.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na Achileo Kivumbi, Kadhafi Mugumya, na Smart Wakabi.


