Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amepongeza shambulio la kushtukiza lililolenga viwanja kadhaa vya ndege vya kijeshi vya Urusi, operesheni iliyopangwa na idara ya ujasusi ya Ukraine, SBU.
Zelenskyy alisema kupitia mtandao wa X:
“Watu wetu walioshiriki kupanga operesheni hii waliondolewa katika ardhi ya Urusi kwa wakati unaofaa.”
Rais huyo wa Ukraine alimalizia ujumbe wake akisema:
“Urusi ilianzisha vita hii, ni Urusi inayopaswa kuimaliza.”
Uwanja mmoja wa ndege wa kijeshi wa Urusi ulivamiwa na ndege zisizo na rubani (drones) kutoka Ukraine katika shambulio lililoratibiwa kwa pamoja, ambapo ripoti zinasema zaidi ya ndege 40 za kijeshi na za upelelezi ziliharibiwa.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilielezea mashambulizi haya kama vitendo vya kigaidi vilivyolenga maeneo ya Ivanovo, Ryazan, Amur, Murmansk na Irkutsk.


