Waandishi wa habari nchini Burundi wameonywa kuwa kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) kunaweza kupelekea kifungo cha miaka 5 hadi 10 pamoja na faini ya milioni 4 za faranga za Burundi, kama alivyoeleza msemaji wa CENI, François Bizimana.
Waandishi wametakiwa kuepuka habari za uongo, uchochezi wa chuki, au taarifa zinazoweza kuwavunja moyo Waburundi wakati wa kipindi hiki cha uchaguzi kilichoanza Alhamisi, tarehe 5 Julai 2025.
Katika kikao kilichofanyika tarehe 2 Juni 2025, Waziri wa Habari, Léocadie Ndacayisaba, kwa kushirikiana na viongozi wa CENI, walikutana kuchagua waandishi watakaoingia katika mtandao wa redio utakaoripoti juu ya mwenendo wa uchaguzi kote nchini.
Katika kikao hicho, Waziri Ndacayisaba aliwaonya waandishi wa habari wasitangaze chochote bila uhakika wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Msemaji wa CENI, François Bizimana, alikumbusha kuwa kifungu cha 239 cha sheria ya uchaguzi kinakataza yeyote kutangaza matokeo kabla ya CENI, na anayefanya hivyo atafungwa miaka 5 hadi 10 na kutozwa faini ya milioni 4 za FBu.
Mitandao ya redio 29, televisheni na vyombo vya habari 30 vya mtandaoni ndivyo vilivyopewa ruhusa ya kufuatilia na kuripoti kuhusu uchaguzi. Taarifa zao zitarushwa moja kwa moja (live) kupitia redio ya taifa.


