Nemanja Matic, aliyekuwa mchezaji wa Manchester United na sasa anayechezea klabu ya Lyon nchini Ufaransa, amefungiwa mechi mbili kwa kuficha alama ya rangi ya upinde wa mvua ya LGBTQ+ kwenye jezi yake wakati wa mechi ya mwisho ya Ligue 1 dhidi ya Angers.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36, ambaye anaripotiwa kuwa mshiriki wa Kanisa la Orthodox la Serbia, alikataa kushiriki katika kampeni ya Ligue 1 iliyolenga kupinga ubaguzi wa kijinsia na kuunga mkono haki za LGBTQ+, ambapo wachezaji walitakiwa kuvaa rangi hizo kuonyesha mshikamano.
Mchezaji mwingine, Ahmed Hassan wa Le Havre, pia alifungiwa mechi mbili kwa kosa kama hilo. Hata hivyo, Mostafa Mohamed wa Nantes, ambaye alikataa kucheza mechi hiyo kabisa, hakuchukuliwa hatua yoyote.
Shirikisho la ligi ya Ligue 1 lilitangaza kuwa Matic na Hassan pia wametakiwa kushiriki katika kampeni ya kuhamasisha mapambano dhidi ya chuki na ubaguzi wa kijinsia kwenye soka.
Kampeni hii imetekelezwa mara tano hadi sasa, lakini kila mwaka baadhi ya wachezaji huipinga, mara nyingi kutokana na imani zao za kidini.
Matic, ambaye aliwahi kushinda Premier League mara mbili akiwa Chelsea, atakosa mechi mbili za kwanza za msimu ujao, baada ya kusaidia Lyon kufuzu kwa Europa League.


