Hali ya uhasama inazidi kuwa mbaya kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na bilionea Elon Musk, baada ya Musk aliyekuwa rafiki wa karibu wake kukosoa sheria ya bajeti iliyopitishwa hivi karibuni.
Uhusiano wao ulikuwa tayari na madoadoa tangu Musk alipojiuzulu kama kiongozi wa shirika la serikali linalosimamia matumizi ya fedha (DOGE) na kurejea katika biashara zake binafsi.
Mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi baada ya utawala wa Trump kuidhinisha ruzuku ya kodi kwa magari ya umeme — eneo ambalo Musk amekuwa akiwekeza kupitia kampuni ya Tesla.
Ruzuku hiyo ilimsaidia Musk kuuza magari mengi zaidi kwa kuwa ushuru ulikuwa mdogo. Baada ya kutambua hilo, Musk alijaribu kushawishi wabunge kuikataa sheria hiyo, lakini hakufanikiwa.
Hivi majuzi, Musk alikosoa sheria hiyo ya bajeti akisema inalenga “kuangamiza Marekani” na kumtaka Trump kushinikiza Maseneta wa Republican kuifuta.
Akizungumza na kituo cha CBS, Musk alimshtumu Trump kwa kumsaliti na kulalamikia matumizi makubwa ya fedha, hasa ruzuku, akisema zinazidisha nakisi ya bajeti ya taifa.
Alisema: “Sheria inaweza kuwa kubwa au nzuri, lakini siyo vyote kwa wakati mmoja.”
Alhamisi, wakati Trump alipokuwa akimpokea Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, alitetea sheria hiyo na kusema ni ya maana sana kwa ahadi zake kwa Wamarekani.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa “aliumia sana” kwa sababu ya Musk, na kwamba uhusiano wao hautarudi kuwa kama zamani.
Trump alisema: “Nilishtuka. Nilihuzunika sana kwa sababu Elon alielewa yaliyomo kwenye sheria hiyo kuliko mtu yeyote.”
Trump pia alidokeza kwamba huenda Musk ana “tatizo.”
Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alimtuhumu Musk kwa “kupoteza akili” kutokana na uamuzi wake kuhusu magari ya umeme.
Musk alijibu kupitia ukurasa wake wa X akimuita Trump “mwenye kutokujua kushukuru,” licha ya kumsaidia kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2024.
Aliandika: “Kama si mimi, Trump angepoteza uchaguzi. Democrats wangekuwa wengi bungeni, na Republicans wangekuwa na viti 49 hadi 51 tu kwenye Seneti. Hana shukrani kabisa!”
Musk pia alisema Trump hajawahi kumwonyesha muswada wa sheria hiyo, akiyaita madai yake kuwa “ya kipuuzi.”
Aliongeza kuwa jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba sheria hiyo ilipitishwa usiku wa manane, na wabunge wakaipigia kura bila hata kuisoma.


